Nafasi Ya Matangazo

October 18, 2016



ISO 9001:2008 CERTIFIED

MASHARTI YA LESENI KWA WAZALISHAJI WA BIDHAA ZINAZOTOZWA
USHURU WA BIDHAA (EXCISE GOODS)
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapenda kuutaarifu umma kuwa, kwa mujibu wa vifungu vya 8 na 16 vya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Sura ya 147, wazalishaji wote wa bidhaa zinazotozwa Ushuru wa Bidhaa na wazalishaji wa malighafi ya kutengenezea spiriti wanatakiwa kusajiliwa na kupewa leseni na Kamishna Mkuu wa TRA kabla ya kuanza uzalishaji. Bidhaa zinazotozwa Ushuru wa Bidhaa zimeainishwa katika jedwali la nne la Sheria husika. Baadhi ya bidhaa hizo ni kama Bia, Sigara, Spiriti, Mvinyo na Vinywaji baridi.
Masharti ya Leseni
1)    Maombi yote yatumwe kwa Kamishna Mkuu kwa kutumia fomu ya maombi ya leseni inayopatikana katika ofisi za TRA au tovuti: www.tra.go.tz

2)    Maombi tofauti yafanywe kama ifuatavyo:
a)    Kwa kila kiwanda ambacho kitatumika kuzalisha bidhaa.  Leseni itatumika kwa kiwanda kilichopewa leseni pekee
b)    Kwa kila aina ya bidhaa itakayozalishwa na leseni itatumika kuzalisha bidhaa husika pekee.

3)    Mmiliki wa leseni hataruhusiwa kuhamisha umiliki wa leseni husika, kubadili kiwanda au kuzalisha bidhaa tofauti katika kiwanda kilichopewa leseni bila kufanya maombi na kuruhusiwa na Kamishna Mkuu.

4)    Baada ya kupewa leseni, mzalishaji anatakiwa kumjulisha Kamishna Mkuu juu ya tarehe ya kuanza uzalishaji ndani ya siku 21 tangu uzalishaji huo kuanza.

5)    Pindi bidhaa yoyote inapoamuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge kuanza kutozwa Ushuru wa Bidhaa, mzalishaji wake anapaswa kumjulisha Kamishna Mkuu na kuomba leseni ya uzalishaji ndani ya siku 21 baada ya bidhaa husika kuanza kutozwa Ushuru wa Bidhaa.

6)    Leseni ya uzalishaji itakwisha muda wake kila tarehe 31 Disemba ya mwaka ambapo mmiliki atatakiwa kuomba leseni mpya.

7)    Wazalishaji wa spiriti yenye vionjo na isiyo na vionjo (Denatured and Undenatured Spirit) pia wanatakiwa kuomba leseni za uzalishaji kwa Kamishna Mkuu.

Uzalishaji wa bidhaa zinazotozwa Ushuru wa Bidhaa bila ya leseni ni kosa linalopelekea adhabu ya faini au kifungo au faini na kifungo ikiwa ni pamoja na kutaifishwa kwa mitambo na bidhaa zote zilizohusika katika utendaji wa kosa hili. Wazalishaji wote wanaaswa kumiliki leseni halali katika wakati wote wa uzalishaji na TRA kwa kushirikiana na wadau wengine wataendesha ukaguzi endelevu kuhakiki matakwa haya ya sheria.
 Waombaji wanatakiwa kufanya maombi katika ofisi yoyote ya TRA ambako viwanda husika vinapatikana ili kuepuka adhabu kali zinazotokana na ukiukwaji wa matakwa haya ya sheria.
 “Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
 Limetolewa na:
Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi
TRA-Makao Makuu
Dar es Salaam
Posted by MROKI On Tuesday, October 18, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo