Nafasi Ya Matangazo

March 13, 2017



Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Saruji Tanga (TCPLC), Diana Malambugi (wa pili kulia), na Meneja Mawasiliano na Mahusiano ya Nje wa Kampuni hiyo, Mtanga Noor (kulia), pamoja na baadhi ya wanawawake wafanyakazi wa Kampuni ya Saruji Tanga pamoja na wake wa wafanyakazi, wakishiriki mbio za mzoezi kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani zilizoanza eneo la Kange na kumalizikia katika kiwanda cha kampuni hiyo, Pongwe, nje kidogo ya mji wa Tanga mwishoni mwa wiki.
*************
WITO umetolewa kwa wafanyakazi wanawake nchini kuwa na utaratibu wa kupima afya zao kwani mwanamke mwenye afya bora ndiye atakayeweza kumudu vyema majukumu yake mahali pa kazi hivyo kuongeza idadi kubwa ya wafanyakazi wanawake katika Tanzania ya viwanda.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Amina Mchalaganya wakati wa sherehe za maadihimisho ya Siku ya Wanawake Duniani zilizoandaliwa na kampuni ya Saruji Tanga (TCPLC) na kufanyika kiwandani hapo, Pongwe Tanga mwishoni mwa wiki.

Alisema wanawake hawana budi kuwa mstari wa mbele katika kupima afya zao mara kwa mara hususan dhidi ya magonjwa ya saratani yanayotishia afya za wanawake wengi hivyo kuathiri kiwango cha cha uzalishaji mali.

“Natoa wito kwa wanawake wa Tanga Cement pamoja na wanawake wote wa Mkoa wa Tanga kujitokeza kupima afya  hasa saratani ya shingo ya kizazi katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo tatizo  linaongoza kuathiri afya za wanawake wengi mkoani humu”, alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo Meneja Mawasiliano na Mahusiano ya Nje wa kampuni hiyo, Bi. Mtanga Noor alisema wameazimia kudhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kufanya matembezi na kupima afya zao kuunga mkono wito wa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwamba tufanye mazoezi kuepuka magonjwa ya kumbukiza.

“Mwanamke mwenye afya ndio mchapa kazi, mwanamke mwenye afya ndiye atakayehakikisha familia yake ina afya, familia ikiwa na afya taifa zima litakuwa na afya na watu tutaweza kuchapa kazi”, alisema.

Akizungumzia ushiriki wa wafanyakazi wanawake katika shughuli za uzalishaji kiwandani hapo Bi. Mtanga alisema kama ambavyo watu wangetegemea kuona idadi ndogo ya wanawake wakifanya kazi katika kiwanda cha kuzalishaji saruji kwao ni tofauti kwani wapo wanawake wengi wanaofanya kazi katika idara za uhandisi, migodini na katika utawala.

Pamoja na hayo meneja mahusiano huyo alitoa wito kwa wazazi wawahamasishe watoto wao wasiogope kusoma masomo ya sayansi kwani baadhi yao huwaandaa watoto wao ili waje wafanye kazi wanazoona ni nyepesi nyepesi pamoja na kuwa tayari wapo wanawake wahandisi, marubani, madaktari lakini akasema bado idadi yao ni ndogo.

Tanzania iliungana na nchi mbalimbali duniani kote kuadhimisha Siku ya Wanawake huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Chochea Mabadiliko kuleta Usawa wa Kijinsia’.
Posted by MROKI On Monday, March 13, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo