Nafasi Ya Matangazo

July 31, 2017



Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dk. Harison Mwakyembe (wa tatu kulia) akikabidhi bendera ya taifa kwa wanariadha wa Timu ya Taifa ya Tanzania itakayoshiriki mashindano ya riadha ya Dunia yatakayofanyika jijini London wiki hii. Timu hiyo yenye wanariadha nane ambapo watano kati yao wanashiriki mbio ndefu za Marathon, imeondoka usiku wa leo kuelekea jijini London. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Dk Omar Singo, Rais wa Chama cha Riadha nchini Anthony Mtaka, K Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania ambao ni wadhamini wakuu wa kambi ya maandalizi ya timu hiyo na aliyemshika mkono Waziri ni Mwanariadha Alphonce Simbu.
 ************
Timu ya taifa ya Riadha itakayoshiriki mashindano ya riadha ya Dunia yanayoanza wiki hii jijini London Uingereza imeagwa na kukabidhiwa rasmi bendera ya Taifa ikiwa ni ishara ya kuwa wawakilishi maalum wa nchi yetu katika mashindano hayo makubwa.

Timu hiyo yenye jumla ya wachezaji nane iliagwa jana na Waziri wa Habari, utamaduni Sanaa na Michezo Harison Mwakyembe katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na maafisa na wadau mbalimbali akiwemo Rais wa chama cha Riadha Tanzania Anthony Mtaka, Mkurugenzi wa Michezo Dr. Omar Singo na Maharage Chande - Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania ambao ni wadhamini wakuu wa timu hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Waziri Mwakyembe alisema Wizara yake iko bega kwa bega na wadau wa michezo hapa nchini katika kuhakikisha kuwa tunapiga hatua katika sekta hiyo na kuifanya moja ya vyanzo vikubwa vya mapato kwa wanamichezo wetu. Amesema serikali imejizatiti kikamilikatika kuratibu na kurasimisha michezo hapa nchini ili wanamichezo watambue kuwa hiyo ni kazi tena ya heshima na yenye malipo makubwa.

Waziri mwakyembe pia alionyeshwa kuridhishwa kwakwe na viwango vya wachezaji na kueleza Imani yake kubwa kuwa wataweza kutuletea ushindi. 

“Kwanza kabisa nimetiwa moyo sana na ari ya vijana waliyonayo na kama mlivyoona na kusikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari, vijana hawa wamepikwa vizuri na wana ari, moyo na uzalendo mkubwa na kilicho mbele yao ni kitu kimoja tu, kupambana kufa na kupona na kurudi na medali”. Alisema Waziri na kuongeza “Nilipoangalia viwango vya vijana wa timu yetu ya taifa nilipata faraja sana. Kwani vijana wote hawa wana viwango vya kimataifa na ndiyo sababu wakapata tiketi ya kushiriki michuano hii ya dunia. Hili siyo suala dogo na napenda niwapongeze sana”

Waziri pia ameipongeza kampuni ya Multichoice Tanzania kwa udhamini wake mkubwa katika maandalizi ya timu hiyo ambapo kampuni hiyo ilikuwa mdau mkubwa katika kufanikisha mafunzo katika kambi hiyo. 

“Sote tunafahamu kuwa katika mchezo wowote ule duniani, mazoezi na maandalizi ni kitu cha msingi sana. Kwa kweli, hapa ni lazima nitoe shukrani za kipekee kwa wenzetu, wadau wa michezo Multichoice Tanzania (DStv) kwa jitihada kubwa walizozifanya katika kuhakikisha kuwa timu yetu hii inafanikiwa kufanya mazoezi na maandalizi kwa ajili ya mashindano haya. Ndugu zetu wa DStv wamejitoa kikamilifu na ndio wadau wakuu walioshiriki katika kuisaidia kambi ya timu yetu iliyokuwa kule Ilboru Arusha. Huu ni uzalendo wa hali ya juu kabisa na ninaomba wadau wengine wasisite kushirikiana nasi katika kuimarisha michezo na Sanaa hapa nchini” Alisema Waziri.

Naye Rais wa chama cha riadha Tanzania Anthony Mtaka, amesema kuwa mbali na jitihada kubwa zinazofanywa na chama hicho bado zipo changamoto nyingi ambazo zinahitaji nguvu za pamoja ili kuhakikisha kuwa riadha inaenda mbele. Amesema kuwa kwa kutambua hilio na kwa kutambua umuhimu wa wadau mbalimbali, wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu sana na wadhamini pamoja na majeshi mbalimbali kama vile JKT na JW ambapo wanariadha wengi wanatoka.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande amesema kuwa  kampuni yake ina dhamira endelevu ya kuibua na kuinua vipaji hapa nchini na ndiyo sababu wakaamua kusaidia katika maandalizi ya timu. “Tumefadhili kwa kiasi kikubwa kambi ya timu iliyokuwa Ilboru Arusha na pia kuahakikisha kuwa timu inawasili Dar na kujiandaa na safari ya London” alisema Maharage na kuongeza kuwa “Tumekuwa tukimdhamini Balozi wetu Alphonce Simbu kwa mwaka mzima sasa. Matokeo ya nguvu zetu tumeyaona. Ametwaa medali ya dhahabu Mumbai Marathon mapema mwaka huu. Na pia amevunja rekodi yake London Marathon. Sasa ni miongoni mwa wakimbiaji wa kutegemewa hapa nchini”. 

“Tumeamua kushiriki kikamilifu kukuza riadha ili kutuwezesha kama taifa kuwa na wigo mpana wa ushindi kwenye mashindano ya kimataifa. Tuna ndoto ya kutaka kuona na kuusikia wimbo wetu wa taifa katika mashindano ya Olmpic. Tumeanza, tumeona matunda, tutaendelea na kuhakikisha ndoto hii inatimia”. Alisisitiza Maharage.

Maharage pia amesema mbali na udhamini huo, DStv inanawahakikisha watanzania kuona na kuwa sehemu ya walimwengu wenye bahati ya kuona mashindano makubwa moja kwa moja. “Zamani kulikuwa ni mambo ya kusimuliwa simuliwa tu… sasa DStv, hatutaki watanzania wasimuliwe yaliyojiri kwenye duru za michezo ulimwenguni… waone wenyewe. Kwa jitihada kubwa tumefanikiwa kuwezesha michuano hiii kuonekana katika vifurushi vyote vya DStv. 

Tutazame tuwaone vijana wetu tushangilie ushindi wetu moja kwa moja bila chenga!” alisema Mkurugenzi huyo na kukumbusha kuwa DStv ilionyesha mubashara Mumbai Marathon tukamuona Simbu akishinda, DStv ikaonyesha  Mubashara London Marathon, tukaona Simbu akivunja rekodi yake, na kwa mara nyingine tena DStv itaonyesha mubashara Mashindano haya ya Dunia, ambapo bila shaka kwa timu tuliyonayo, tutashuhudia tukikwapua medali kedekede na kuliletea taifa letu sifa kubwa.

Akizungumza mara tu baada ya timu yao kukabidhiwa bendera, mmoja wa wanariadha hao Alphonce Simbu anayeshiriki mbio ndefu za kilmita 42 amesema kuwa wao wamejiandaa kikamilifu na wanajua wanabeba dhamana kubwa kwa watanzania wote. Hivyo watahakikisha kuwa wanapambana na kuleta medali nyumbani.

Amesema wamejiandaa vizuri na makocha wamefanya kazi kubwa hivyo kilichobaki ni kwa watanzania wote kuwaombea na pia kuhakikisha wanawashuhudia moja kwa moja kupitia DStv kuona jinsi wanavyotuwakilisha kwenye mashindano hayo.

Jumla ya wanariada watano watashiriki mbio za kilomita 42 ambao na Aplphonce Simbu  mwenye rekodi ya 2:09.10- aliyoiweka hivi karibuni katika London Marathon 2017; Ezekiel Jafari Ng’imba 2:11.55- Hannover Marathon 2017; Stephano Huche Gwandu –  2:14.18 – Tunis Marathon; Sara Ramadhani Mkera 2:33.08- Dusseldorf Marathon 2017 na Magdalena Crispin Shauri 2:33.28 Hamburg Marathon 2017.

Wakimbiaji watatu waliosalia wanashiriki mbio fupi ambapo Gabriel Gerald Geay anashiriki mita 5,000; Emanuel Giniki Gisamoda pia mita  5000 na Failuna  Abdi  Matanga wa mita 10,000.
Mashindano hayo yataanza rasmi tarehe 4 Agosti na yataendelea kwa takriban siku 10.
Posted by MROKI On Monday, July 31, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo